Mtume Wangu Mpendwa

TUKIO LA BIR MAUNA

Katika mwezi wa Safar wa mwaka huo huo, Abu Bara Amir bin Malik, kiongozi wa Bani Amir katika eneo la Najd la Arabia, alikuja Madina. Alimtembelea Bwana wetu Mtume Mtukufu (sallallahu alayhi wasallam). Bwana wetu Mtume naye alimweleza Uislamu na kumshauri asilimu. Abu Bara hakusilimu, lakini alisema kwamba Uislamu ni dini nzuri na tukufu. Zaidi ya hayo, aliomba Bwana wetu Mtume atume huko baadhi ya Masahaba watukufu ili Uislamu uenee Najd. Mtume wetu mpendwa alisema: “Nawahofia wale nitakaowatuma kutokana na watu wa Najd!” Amir alisema: “Mimi nitawachukua chini ya ulinzi wangu. Hapo hakuna atakayeweza kuwadhuru.”

Bwana wa walimwengu aliikubali ahadi hii thabiti, akaandaa ujumbe wa watu sabini kutoka miongoni mwa Ashab as-Suffa. Hawa walikuwa wakisoma Quran tukufu usiku. Wote walikuwa mahafidhi (Waislamu waliohifadhi Quran tukufu kwa moyo). Waliitwa Ashab al-qurra. Majina ya baadhi yao ni haya: Amir bin Fahr, Amr bin Dhamri, Atiyya bin Abdullah, Anas bin Muawiya, Hakam bin Kaysan, Harith bin Samma, Kaab bin Zayd, Malik bin Thabit, Mundhir bin Amr, Rafi bin Mazil, Said bin Huzam, Salim bin Milhan, Suhayl bin Amir, Tufayl bin Asad na Urwa bin Salt (radhiyallahu taala anhum). Kwa amri ya Rasulullah waliondoka chini ya uongozi wa Hadhrat Mundhir bin Amr. Rasulullah pia aliandikisha barua, akazipeleka kwa viongozi wa Bani Amr na Bani Najd, kila mmoja barua yake.

Abu Bara, akitaka kabila lake lipate heshima ya kusilimu, aliondoka kabla ya Ashab as-Suffa na kufika kwa kabila lake; aliwaarifu kwamba ameuchukua ujumbe chini ya ulinzi wake, na akawaonya mtu yeyote asiwaguse. Wote isipokuwa mpwa wake Amir bin Tufayl walikubali kutowagusa. Amir bin Tufayl, mpwa wa Abu Bara, aliwapa silaha watu wa makabila matatu, akawa kiongozi wao, na akawazingira Masahaba watukufu waliokuja Bir Mauna. Masahaba, waliozingirwa pande zote nne, walishika panga zao na wote walipigana kishujaa hadi tone la mwisho la damu yao. Wote, isipokuwa wawili kati yao, walikunywa sharubati ya kufa shahidi. Hadhrat Amr bin Umayya walimchukua mateka. Na Hadhrat Kaab bin Zayd walimwacha wakidhani amekufa.

Maneno ya mwisho ya Masahaba hawa waliobarikiwa waliokufa mashahidi yalikuwa: “Ewe Mola wetu! Hivi sasa hakuna mwingine isipokuwa Wewe wa kumpa Rasulullah habari za hali yetu. Mfikishie salamu zetu!” Wakati huo Jibril alaihis-salaam, akiwa na huzuni kubwa mno, alikuja kwa Bwana wetu Mtume, akamfikishia salamu zao na kusema: “Wao wamekutana na Allahu taala. Allahu taala yuko radhi nao, nao wako radhi na Allahu taala.”

Mtume wetu mpendwa, baada ya kujibu: “Wa alaihimus-salaam,” aliwageukia Masahaba Wake watukufu kwa huzuni kubwa, akawaeleza yaliyotokea kwa maneno haya: “Ndugu zenu wamekutana na washirikina. Washirikina wamewakatakata na kuwatoboa kwa mikuki yao…”

“Wao (mashahidi wa Bir Mauna) wamekutana na Allahu taala. Allahu taala yuko radhi nao, nao wako radhi na Allahu taala” Hadithi sharif

Tukio la Bir Mauna

Roho Yako ni nukta ya nuru ya Allah, ya Rasulallah, Uzuri Wako huongeza furaha na hufungua nyoyo, ya Rasulallah, Waislamu wote wanajua kwamba kudhihiri kwa dhati Yako, alama ya rehema, Kuliondoa giza lote la ukafiri, ya Rasulallah. Katika bustani ya waridi ya utume, dhati Yako ni mti wa waridi, Na hata hivyo Wewe ndiwe mche wa mwisho aliouotesha Allah, ya Rasulallah, Fanya ukarimu, ewe uliye hoja tukufu kabisa ya Mola, Wingi wa fadhila Zako ndio dawa ya dhiki ya Najib, ya Rasulallah. SULTANI AHMAD III (NAJIB)

Katika tukio hili, Hadhrat Amir bin Fuhayra alipokuwa akipigana na adui, mtu mmoja aitwaye Jabbar alimchoma mkuki mgongoni. Wakati huo Hadhrat Amir alisema: “Wallahi, nimeipata Pepo!” Kisha mwili wake ulipandishwa mbinguni mbele ya macho ya Jabbar na washirikina wengine. Wote walishangazwa na hali hii, lakini miongoni mwao ni Jabbar tu, aliyemuua, aliyesilimu.

Bwana wetu Mtume alihuzunika sana kwa sababu ya matukio ya Raji na Bir Mauna. Kwa mwezi mzima, baada ya kila sala, aliyaombea balaa makabila yaliyofanya matukio haya ya kuhuzunisha. Allahu taala aliikubali dua ya Mtume Wake. Aliyapelekea makabila hayo ukame wa kutisha na njaa. Baadaye watu mia saba kati yao walikufa kwa ugonjwa wa kuambukiza.1

Wewe ni tabibu wa walimwengu, nami ni mgonjwa sana wa moyo,
Nimekuletea moyo wangu nikitumaini kupata shifaa.
Mgongoni mwangu mna mlima wa dhambi, na uso wangu umepauka kama nyasi kavu kwa hofu,
Lakini nimejaa matumaini – nimezileta hapa dhambi zangu ili zifutwe.
Ewe Bwana wa walimwengu! Nakupenda na nimekustaajabia;
Usiku na mchana nalia kwa kutengana Nawe.
Rehema Yako kubwa ni maji ya uhai, nami nina kiu;
Nisipopata hata tone lake moja, nitakufa na kutoa roho.
Kumsifu Yeye kwa tabia Yake ni juhudi ya bure,
Kumweleza kwa maneno ni vigumu zaidi.
Yeye ni mwingi wa kusamehe, mkarimu na mpaji mno: lulu hutoka majini,
Johari hutoka jiweni, waridi hutoka mwibani.
Ikiwa jua linatoa nuru, ni kutokana na nuru Zake,
Tone la umande juu ya waridi linatoka katika uso Wake wa waridi.
Kumweleza Yeye ni jambo lililo juu kuliko haya,
Lakini nikisema zaidi, wageni watakanusha.
Inawezekana kuuweka ulimwengu wote ndani ya chembe moja ya vumbi,
Kumweleza Yeye kwa maneno ni vigumu kwangu kuliko hilo.
Mawlana Khalid al-Baghdadi

“Wallahi, nimeipata Pepo!” Amir bin Fuhayra (radhiyallahu anhu)

Vita vya Bani Nadir