NGUZO ZA UISLAMU
Kwa wale walioingia katika dini ya Uislamu, yaani Waislamu, kuna majukumu matano ya fardhi ambayo ni lazima kabisa kuyatekeleza. Nayo ni:
1. Nguzo ya kwanza kati ya nguzo tano za Uislamu ni kutamka Kalima ash-shahada, yaani kusema: “Ashhadu an la ilaha illallah wa ashhadu anna Muhammadan abduhu wa rasuluhu”. Kwa maneno mengine, mtu mwenye akili timamu, aliyebaleghe na anayeweza kuzungumza, ni lazima aseme kwa ulimi wake, na aamini kwa moyo wake kwa uthabiti na yakini: “Ardhini na mbinguni hakuna kitu chochote wala mtu yeyote, isipokuwa Allahu taala, mwenye haki ya kuabudiwa na anayestahiki kuabudiwa. Mwabudiwa (mabud) wa kweli ni Allahu taala peke Yake.” Yeye ni Wajib al-wujud. Kila ubora ni Wake. Hana upungufu wowote. Jina Lake ni “Allah”. Na pia: Yeye mwenye uso wenye rangi ya waridi, mweupe na mwekundu, unaong’aa na wenye kupendeza; mwenye nyusi nyeusi na macho meusi, paji la uso pana lililobarikiwa, na tabia njema; ambaye kivuli Chake hakikuanguka ardhini; mwenye maneno matamu; aliyezaliwa Makka katika nchi ya Waarabu, na kwa hiyo huitwa Mwarabu; kutoka katika kizazi cha Hashim – “Muhammad, mwana wa Abdullah, ni mja wa Allahu taala na Rasul Wake, yaani Mtume Wake.” Yeye ni mwana wa Hadhrat Amina binti Wahb. Na, alhamdulillah, Yeye pia ni Mtume wetu mpendwa (sallallahu alayhi wasallam).
2. Nguzo ya pili kati ya nguzo tano za Uislamu ni kusali sala mara tano kila siku, wakati wake unapoingia, kwa kufuata masharti na fardhi zake. Tangu zama za Adam alaihis-salaam, katika kila dini kulikuwa na sala ya wakati mmoja kwa siku. Sala walizozisali wote hao zilikusanywa pamoja na kufanywa fardhi kwetu. Ingawa kusali si sharti la imani, kuamini kwamba sala ni fardhi ni sharti la imani. Kwa kila Mwislamu aliye mukallaf [yaani mwenye akili timamu na aliyebaleghe], kusali sala tano kila siku ni fardhi ayn. Sala tano za kila siku ziliamrishwa usiku wa Miraji. Kabla ya Miraji kulikuwa na sala ya alfajiri na ya alasiri tu.
3. Nguzo ya tatu kati ya nguzo tano za Uislamu ni kutoa zaka ya mali yake. Kilugha, zaka maana yake ni usafi, kusifu, na kuwa katika hali nzuri na njema. Katika Uislamu, zaka ni kwamba mtu mwenye mali ya zaka iliyozidi mahitaji yake na kufikia kiasi maalumu kinachoitwa nisab, atenge sehemu maalumu ya mali yake na awape Waislamu waliotajwa katika Quran tukufu, bila kuwasimbulia. Katika madhehebu yote manne kuna aina nne za mali ya zaka: zaka ya dhahabu na fedha, zaka ya mali ya biashara, zaka ya wanyama wa miguu minne wanaofugwa kwa ajili ya nyama, wanaokula majani malishoni zaidi ya nusu ya mwaka, na zaka ya mazao ya ardhi. Zaka hii ya nne huitwa ushr, nayo hutolewa mara tu mazao yanapovunwa. Zaka nyingine tatu hutolewa mwaka mmoja baada ya mali kufikia kiasi cha nisab.
4. Nguzo ya nne kati ya nguzo tano za Uislamu ni kufunga kila siku ya mwezi mtukufu wa Ramadhani. Kufunga huitwa saumu. Kilugha, saumu maana yake ni kukihifadhi kitu kimoja kutokana na kitu kingine. Katika Uislamu, saumu maana yake ni kwamba mtu, akizingatia masharti yake, na kwa sababu Allahu taala ameamrisha hivyo, ajizuie na mambo matatu kila siku ya mwezi wa Ramadhani. Mambo haya matatu ni kula, kunywa na jimai (tendo la ndoa).
5. Nguzo ya tano kati ya nguzo tano za Uislamu ni kwenda hija mara moja katika umri wake kwa yule mwenye uwezo. Mtu mwenye fedha za kutosha kwenda mji wa Makka al-Mukarrama na kurudi, mbali na mali inayotosha kuwakimu watu wa nyumbani anaowaacha nyuma mpaka atakaporudi, ana fardhi ya kuitufu Kaaba al-Muazzama akiwa katika ihram na kusimama (wuquf) katika uwanja wa Arafat mara moja katika umri wake, ikiwa njia ni salama na mwili ni mzima.
“Katika Quran tukufu kila kitu ambacho waja wanakihitaji kimeelezwa; wasioamini wameonywa kwa adhabu, na waumini wanaotekeleza nguzo za Uislamu wamepewa bishara ya Pepo” Imam Rabbani (rahmatullahi alaih)
Njooni tusali sala, tuondoe kutu nyoyoni,
hakuna kumkaribia Allah bila kusali sala!
Pale sala inaposaliwa, madhambi yote hupukutika,
mwanadamu hawezi kukamilika bila kusali sala!
Katika Quran tukufu Haki ameisifu sala sana,
amesema: “Simpendi mtu asiyesali sala!”
Katika hadithi sharif imesemwa: alama ya imani
haidhihiriki kwa mtu bila kusali sala!
Kuacha sala moja ni katika madhambi makubwa kabisa,
haisamehewi kwa toba bila kuilipa kadha!
Anayeidharau sala hutoka katika imani papo hapo,
hawezi kuwa Mwislamu bila kusali sala!
Sala husafisha moyo na kumzuia mtu na maovu,
huwezi kupata nuru bila kusali sala!
